AVUMILIAYE MPAKA MWISHO NDIYE ATAKAYEOKOKA!

Habari ya uzima mpenzi msomaji wa makala zetu,tunayofuraha kuzidi kuendelea kujifunza pamoja nawe.Siku ya leo ni siku ya pekee kabisa ambayo tunakwenda kuzungumzia habari ya kuvumilia mpaka mwisho.


Kuvumilia ni kule kukabiliana na changamoto zozote unazokutana nazo pasi na kukata tamaa,kurudi nyumba au kukubali kushindwa.
Anayevumilia ni yule asiyekuwa tayari kushindwa licha ya ugumu anaoupitia.


Kuvumilia kuna ukomo tofauti tofauti kulingana na mtu binafsi na ugumu husika anaoupitia.
Kwa uzito uleule wa kazi fulani au changamoto fulani,wapo watu wa makundi yafuatayo kuhusiana na viwango vya uvumilivu wao.


WANAOVUMILIA MUDA MFUPI TU.
Kuna wengine huweza kuvumilia changamoto kwa muda mfupi tu na kukata tamaa au kuchoka kabisa na asiwe tayari kuendelea tena.
Hawa wengi wao wanakuwa bado hawajayakaribia mafanikio kabisa yaani wanapothubutu tu kufanya jambo la kuwapeleka kwenye mafanikio, wakikutana na changamoto hukimbia kana kwamba wanapokimbilia hakuna changamoto.
Hawa wanadhani kufikia kilele cha mafanikio na kuendelea kusonga mbele kunakuja tu bila kupitia ugumu wowote wala kutumia nguvu sana yaani wanafikiri ni suala la mtelemko tu hakuna milima wala miinuko.Kundi hili lina idadi kubwa ya watu.


WANAOVUMILIA MUDA MREFU TU.
Ndio wengine wanauwezo wa kuvumilia kwa muda mrefu sana lakini tatizo hawafiki mwisho hawa wanayakaribia mafanikio lakini wanakata tamaa kabla hawajafanikiwa licha ya kuvumilia muda mrefu sana, wanakata tamaa na kuona hawawezi kuendelea kuvumilia tena kwa kuhisi hata wangeendelea kuvumilia wasingepata matunda tarajiwa.Wanatambua kuhusu milima lakini wanatarajia kuwepo na mtelemko kidogo wapumue ndipo wasonge mbele,inapotokea hawapati mtelemko na wala hawafiki tambarare safari ya kupandisha miinuko tu huwachosha na kuishia njiani licha ya kuvumilia sana.Hapa kuna watu wengi pia japo ni wachache ukilinganisha na kundi la kwanza.Hawa wamekula ng'ombe mzima lakini mkia umewashinda na wamekubali kuuacha!


WANAOVUMILIA MPAKA MWISHO.
Hili ni kundi la watu ambao hawako tayari kukatisha safari zao za kufikia mafanikio ya kweli kwenye maisha yao bila kujali wanapitia ugumu gani ,bila kujali wanakabiliwa na changamoto gani wao wanasonga mbele kwa kuwa wanafahamu fika kuna milima na mabonde,kuna tambarare na mteremko pia hawana hofu hata kama wanapanda milima tu wanahakika watafika kileleni na upande wa pili hautakuwa mlima tena maana yake wataanza kuteremka na huko ndiko mafanikio yalipo.Wanamatumaini na safari yao hawaishii njiani ,hawarudi nyuma wala hawakati tamaa kwa kuwa wameamua kuvumilia hadi wapate kile wanachotaka kwenye maisha yao. Hili kundi lina watu wachache sana ambao wanaweza kuvumilia mpaka mwisho.


Ni hamu yangu sote tujifunze kuwa kundi la tatu ambalo linatupeleka kwenye kilele cha mafanikio tunayoyataka,anza mazoezi leo kuthubutu na kuvumilia mpaka mwisho.
Kuvumilia mpaka mwisho ni kuvumilia mpaka umeona matunda halisi ya uvumulivu wako.Avumiliaye mpaka mwisho ndiye anaekula matunda ya uvumilivu naam ndiye atakayeokoka!


Imeandikwa na Antony Mwakilima
Mawasiliano:    0756-351 462
                              0672-314 874
Email:mwaijox@gmail.com
    
          KWA PAMOJA TUNAWEZA
                           ©2016


Comments

Popular posts from this blog

KIPIMO UNACHOPIMIA WENGINE NDICHO UTAKACHOPIMIWA

HASIRA HASARA