USIANGALIE ULIONAO ANGALIA WATAKAOKUJA

Habari ya siku ya leo mpendwa msomaji wa makala mbalimbali katika blog yetu?ni matumaini yangu kuwa uko vizuri na unaendelea kupambana kuhakikisha unakuwa na maisha unayoyataka lakini kwa ajili ya wengine yaani watu wa kundi lako. Karibu tena tuendelee kuongeza thamani kwenye maisha yetu.

Haijalishi ulikuwa na kundi LA watu au marafiki kiasi gani kwenye maisha yako Jana. Maamuzi yako yatakayoibadilisha kwanza Leo na kuleta kesho mpya yanayo matokeo mawili.

(1) Yanaweza kupelekea kuongezeka kwa marafiki wapya au idadi ya watu wa kundi lako.
Hili likitokea wengi hatuna mashaka wala hatuogopi na tunaona ni kawaida na maisha yanaendelea. Yamkini iko hivi kwa sababu bado unaeleweka yaani hujabadilika umeendelea kuwa yuleyule kila siku hata ukiamua kubadilika unabadilika kidogo sana bila kuathiri maisha ya hilo kundi ulilonalo na pia inawezekana ukaona kawaida kwa sababu kila siku marafiki huongezeka, inabidi utambue sio kawaida ukiona kundi lako linaongezeka ujue unahitaji nguvu zaidi kuweza kuliridhisha au kulifikisha linapotakiwa kwenda. Kwa hiyo usione jambo la kawaida unapoona watu wa kundi lako wameongezeka badala yake tafuta zaidi kuwa bora ili uboreshe na wao.
Huwezi kumpa mtu sabuni na maji afulie nguo zake wakati za kwako ni chafu. Huwezi kumuinua maskini ukiwa maskini!
Ni lazima uwe na ziada(double portion) kwa ajili yako na kundi lako.

(2) Yanaweza kusababisha kundi La watu ulilonalo likapungua.
Matokeo haya yajapo hapa ndipo hofu na mashaka huingia pale unapoona mtu uliyekuwa nae karibu sana uliyemtegemea kwa ushauri, mawazo au maoni kwa kila hatua unayokwenda naye amekula kona wala hataki kufanya tena pamoja nawe. Ndio ukiona hivyo ujue umefanya Kitu cha tofauti,Kitu kilicho nje ya mazoea ya kawaida, Kitu ambacho kitagusa maisha ya wengine na kuyaathiri kinyume na matarajio yao, matokeo kama haya ni ishara ya kuwa umeanza kufanya maisha yako, umeanza kuishi maisha yako. Ukiishi maisha yako unatofautiana na wengine na hapo ndio mwanzo wa mafanikio yako, Lazima ukubali kufanya maamuzi magumu hata kama yatawafukuza wote ubaki peke yako, wewe Fanya ilimladi huvunji sheria wala huingilii Uhuru wa wengine ni kwa ajili yako ni kwa maisha yako Fanya tu marafiki watakuja wengi tena watakaoendana na wewe yaani wenye mtazamo sawa na wewe, wenye malengo kama wewe hivyo usije ukaogopa kufanya maamuzi sahihi yatakayobadili maisha yako kwa sababu unahofia kupoteza marafiki. Acha wapotee yamkini ni marafiki wanafiki wanaofurahia viwango vyako vya maisha viendelee kuwa chini, pengine ni marafiki wasiopenda mafanikio yako, inawezekana wamekuwa marafiki kwako ili waendelee kukufariji ubaki hatua ileile kila siku.

Haijalishi unawaamini kiasi gani inapotokea suala la kufanya maamuzi magumu yatakagobadili mustakabali wa maisha yako unafanya jambo moja 'unaamua tu' bila kujali nani atapungua au kuongezeka kikubwa ni kubadili mwelekeo wa maisha yako kuwa bora zaidi. Kuna wakati umekuwa msaada kwa marafiki ndugu na jamaa zako lakini inapotakiwa ufanye maamuzi yatofauti yaani unafunga misaada uliyokuwa unatoa ,unakuwa bize kuliko kawaida, unapunguza kuwasiliana na wale uliokuwa unawasiliana nao Mara kwa mara bila kupata chochote, unaanza kuyaangalia maisha yako kwa namna ya tofauti hapa lazima waondoke wote ambao walikuwa wanaangalia msaada wako, walioangalia kujali kwako, wale walioangalia kujitoa kwako wataanza kupungua taratibu. Unaweza usielewe sasa hivi lakini unapoamua kusitisha kufanya mambo yote kwa ajili ya wengine ili kuboresha maisha yako na kupanua wigo wakuwasaidia wao na wengine wengi zaidi baadae, uwe na uhakika wengi tu hawatafurahi, hawatakuelewa na hawatakubali wala kuamini kwa wakati huo hadi waone matokeo. Kwa hiyo suala la kujiondoa miongoni mwa marafiki zako ni jambo la kawaida. Inakuhitaji kuwa na maamuzi magumu kuyaboresha maisha yako maana ni hatua itakayowakwaza wengi na kuwaondoa wasiosahihi kwako hata wakati mwingine walio sahihi hawatakuelewa Lakini ndio inabidi usieleweke ili uboreke zaidi.
Kumtegemea MUNGU kuna faida kedekede unapogundua jambo hili na kuyakabidhi maisha yako kwa MUNGU kuna watu hawatakuelewa lakini ndio fungu jema ulilochagua, kuna wakati utathubutu kuanzisha biashara na mtaji ukawa Pesa ambayo wangehitaji uwasaidie na wewe umeitumia huko hawawezi kukuvumilia japo unalenga kuboresha maisha yenu pamoja lakini hawawezi kuona umuhimu wa kushindwa kula vizuri kwa sababu ya biashara yako au mradi wako ambao ni asilimia nusu kwa nusu faida au hasara, nataka nikwambie usiyumbishwe na watu wa kundi lako. Nielewe hivi kila mtu amepewa watu awatoe hatua moja ya maisha waingie hatua nyingine bora zaidi, huwezi kumhudumia mgonjwa kwa kusikiliza matakwa yake, huwezi kumpa mtu mwingine chakula wakati wewe pia unanjaa au huwezi kuwa tayari kumsaidia mwingine unapokuwa unahitaji msaada huohuo kwa kifupi tukilingana hatuwezi kusaidiana lazima ujue kundi lako linataka nini na wewe ufanye nini ili kundi lote lipige hatua!

Kuna wengine sio wa kundi lako acha wapungue watakwamisha tu safari yako buuureee! Yape nafasi mambo yatakoyobadili mfumo wa maisha yako kuwa bora zaidi bila kujali watu wanaokuzunguka watakuonaje itakusaidia!
Angalia watakaokuja kwa sababu ulionao ukianza safari wakiwa wakwako watakufuata, lakini wenye mawazo, malengo na mtazamo sawa na wewe watakuja tu utakapofanya maamuzi magumu na kuanza kuishi kinyume na mazoea!

Imeandikwa na Antony Mwakilima.
Mawasiliano:     0756 351 462
                            0672 314 874
email:     mwaijox@gmail.com

       TAFAKARI BADILI MTAZAMO
                           ©2017

Comments

Popular posts from this blog

AVUMILIAYE MPAKA MWISHO NDIYE ATAKAYEOKOKA!

KIPIMO UNACHOPIMIA WENGINE NDICHO UTAKACHOPIMIWA

HASIRA HASARA