THAMANI UNAYOTOA SI SAWA NA WANAYOIPOKEA

Ninayofuraha kukualika tena rafiki mpendwa mfuatiliaji wa makala zetu,ni imani yangu kuwa wewe ni mzima wa afya kabisa na unaendelea vizuri katika yote unayojishughurisha nayo kuhahakikisha unafikia mafanikio yale uyatakayo.


Ni siku nzuri tena ninayotaka tushirikishane juu ya unavyotoa kwa wengine na namna ambavyo wanavipokea na ukubwa ambao wanavichukulia vile unavyovitoa.
Ni mara nyingi sana watu wengi wamekuwa wanashindwa kutoa kwa sababu wanadhani kwamba kila anayepewa anahitaji kikubwa ili aitambue thamani ya mtoaji.


Nimekuwa shahidi wa jambo hili ndio maana nimeamua nikushirikishe ili tupate ufahamu huu wa ajabu ,mimi nimejifunza kwamba inapofikia hatua ya kumfanyia mtu kitu watu wengi tumekuwa na kasumba ya kujithaminisha kwa kuangalia kazi au shughuri unazofanya na jinsi ambavyo mtu huyo unayetaka kutoa kwake mnaheshimiana kiasi gani? au atakuchukuliaje ukitoa kwake hicho unachotaka kutoa?
Yawezekana umefikia hatua hii kwa sababu unadhani unachotaka kutoa ni kidogo sana na kwamba ataona umemdharau au kumvunjia heshima unayekwenda kumtolea,nikwambie kitu,


Mama yangu aliwahi kuniambia 'hata kama unachokidogo usisubiri mpaka uwe na kikubwa ndipo umkumbuke mtu au umsaidie au utoe kama mimi ukinitumia vocha au elfu kumi tu hata kama kazi yako inakuingizia pesa nyingi nitakushukuru na kukuombea baraka hivyo ndivyo utakavyokuwa unafanikiwa zaidi'  hayo maneno niliambiwa na mama yangu na hicho ni kitu watu wengi hawajakitambua wamekuwa wanataka wajikusanye hadi wapate pesa nyingi au vitu vingi ndio wawapelekee wanaohitaji au ndio watoe kuwasaidia wengine.
Nilipomuuliza kwa nini amesema maneno hayo alinambia,wakati mwingine mtu anakuwa hajatarajia kupokea hata hicho kidogo unachodhani hakitamfaa kwa hiyo unapompa kwa wakati ambao hakutegemea kupokea chochote anafurahi na kukushukuru hata kama ni vocha ya elfu moja atakubariki kwa kuwa umempa nafasi ya kuwakumbuka wengine pale atakapo wapigia na kuwajulia hali zao watafurahi na kumshukuru yeye na hivyo hatoacha kukuombea mafanikio zaidi wewe japo ulidhani elfu moja haiwezi kupokelewa kwa furaha namna hiyo.


Bibi yangu pia aliwahi kuniambia jambo kubwa analolipenda yeye ni kumsalimia au kumjulia hali.Ile kwamba umempigia simu ukamsalimia hata kama hajakuona anafarijika na kujiona anathaminiwa na wewe na hivyo furaha yake huamua amani juu ya maisha yako maana yake badala ya yeye kunung'unika kwa sababu yako sasa anafurahi juu yako.
Mara nyingine manung'uniko ya wale uliowatendea ubaya hulaani maisha yako,usiipe nafasi laana itokanayo na manung'uniko hasa kwa watu waliokaribu na wewe,hilo jambo unaloliona lina thamani ndogo litende vivyo hivyo maana wapo watu wanaolingoja litendeke wakubariki kwa kuwa linathamani kubwa kwenye maisha yao.
Kuna watu wameshindwa hata kutembelea ndugu zao ,rafiki zao,wazazi wao kwa sababu wamekosa kitu cha kuwapelekea kama zawadi wakasahau kuwa ile salamu tu inatosha kuwafanya ndugu zako wakufurahie. Ni rahisi kufanikiwa kama unafurahiwa na watu maana hawatakunenea mabaya watakubariki kila hatua unayoiendea .


Usiogope kufanya jambo lolote jema kwa wengine kwa sababu unadhani ni jambo dogo.Usifunge baraka zako au njia za mafanikio yako kwa kutokutoa ukihofia uchache wa vile ulivyonavyo usingoje uwe na vingi ndipo utoe kwa kuwa hivyo vichache vina thamani kubwa kwa unaoenda kuwatendea.


Imeandikwa na Antony Mwakilima
mawasiliano;      0756-351 462
                            0672-314 874
email;mwaijox@gmail.com


      
           KWA PAMOJA TUNAWEZA
                           ©2016


Comments

Popular posts from this blog

AVUMILIAYE MPAKA MWISHO NDIYE ATAKAYEOKOKA!

KIPIMO UNACHOPIMIA WENGINE NDICHO UTAKACHOPIMIWA

HASIRA HASARA